Monday, 22 August 2016

KILIMO CHA KAROTI

          




Karoti ni zao ambalo hulimwa zaidi katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Morogoro, Iringa, Mbeya na Kagera. Ndugu msomaji maeneo tajwa hapo juu hulimwa zaidi kwa maana hiyo karoti inaweza kulimwa katika maeneo mengine pia yenye sifa zinazo kalibiana na hiyo mikoa.  hustawi vizuri kwenye sehemu zenye joto la wastani (nyuzi joto 15 hadi 27 za Sentigredi).
Zao hili hutumika kama kiungo katika mapishi ya vyakula mbalimbali. Huweza kutafunwa mbichi au kuchanganywa kwenye kachumbari. Karoti zina vitamin A, C na madini aina ya chuma.
Karoti hupandwa moja kwa moja shambani katika matuta au sesa. Kiasi cha gramu 80 (sawa na vijiko vidogo vya chai 16) kinatosha kupanda eneo la mita za mraba 100. Eka moja huhitaji kilo 3.2 za mbegu.

Hakikisha mbegu unazozipanda zina uwezo wa kuota kwa kuzifikicha. Mbegu zenye uwezo wa kuota hutoa harufu kali unapozifikicha. Zilizopoteza uwezo wa kuota huwa hazitoi harufu yoyote. Ili mbegu ziote haraka ziloweke katika maji kwa muda wa saa 24. Baada ya hapo changanya mbegu hizo na mchanga, kwa kiasi kinacholingana ili kupata mtawanyiko mzuri wa mbegu wakati wa kupanda/kusia.
 Maandalizi ya shamba
Ø Lima shamba kwa trekta, kwa ng’ombe ama kwa jembe la mkono kwa kina cha sentimita 30 hadi 45
Ø Andaa matuta yenye mwinuko na kimo cha sentimita 30-40, na upana wa mita 1 na mita 1.5 kutoka katikati ya tuta na tuta. Tengeneza mifereji midogo ya kusiha mbegu za karoti yenye umbali wa sentimita 15- 20, mifereji minne kwa tuta
Ø Weka mbegu katika chupa ndogo ya mililita 100 na toboa kidogo mfuniko
Ø Sia mbegu katika mifereji ya kupandia kwa kutikisa chupa yenye mbegu
Ø Funika mbegu kwa kutumia mboji au mchanga
Ø Nyunyiza maji ya kutosha
Ø Funika tuta na plastiki nyeusi
Ø Kandamiza plastiki kwa pembeni na kwa mabonge ya udongo ili isipeperushwe na upepo
Ø Mbegu huota baada ya siku 3-5 kutegemea na hali ya hewa
Ø Zingatia kukagua shamba mara tatu kwa siku.
Ø Ondoa plastiki mara moja pindi utakapoona mbegu moja tu iliyoota
Ø Kuchelewa kuondoa plastiki husababisha miche inayoota kufa kwa kuunguzwa na joto lililo katika plastiki
Palizi
Palilia shamba mara kwa mara ili kuhakikisha shamba halina magugu
Magugu hudhibitiwa kwa palizi ya jembe, kung’oa kwa mkono ama matumizi ya viuagugu
Matumizi ya viuatilifu yafanyike kila baada ya wiki mbili
Mbolea
Tumia mbolea ya DAP wakati wa kupanda, CAN ama SA wiki tatu baadaye na kisha tumia NPK wiki sita baada ya kupanda. Matumizi ya mbolea za maji yafanyike kila baada ya wiki mbili kutegemea na mahitaji

Magonjwa:
· Madoajani (Leaf Spot):
Ugonjwa huu husababishwa na ukungu na hutokea wakati karoti zina urefu wa sentimita 13 mpaka 15. Hushambulia majani na kuyafanya yawe na madoa yenye rangi nyeusi iliyochanganyika na kijivu au kahawia. Sehemu zinazozunguka madoa haya hubadilika rangi na kuwa njano. Ugonjwa ukizidi majani hukauka. Zuia ugonjwa huu kwa kunyunyizia dawa za ukungu kama vile Dithane-M 45, Blitox, Copperhydroxide (Kocide), Copper Oxychloride, Cupric Hydroxide (Champion), Antrocol, Topsin M- 70% na Ridomil.
· Kuoza Mizizi (Sclerotinia Rot).
Ugonjwa huu husababishwa na ukungu na hushambulia mizizi namajani. Dalili zake ni kuoza kwa mizizi na majani. Baadaye sehemu hizi hufunikwa na uyoga mweupe. Kwenye uyoga huu huota siklerotia kubwa zenye rangi nyeusi.
Zuia ugonjwa huu kwa kuzingatia yafuatayo:-
- Epuka kustawisha karoti kwenye maeneo yaliyoshambuliwa na ugonjwa huu.
- Nyunyuzia dawa za ukungu kama vile Dithane M- 45, Blitox, Topsin - M 70% na Ridomil.
· Madoa Meusi (Black Leaf Spot):
Huu pia ni ugonjwa wa ukungu unaoshambulia majani na mizizi. Majani yaliyoshambuliwa huwa na rangi ya manjano ambayo baadaye hubadilika na kuwa kahawia. Mizizi huwa na madoa meusi yaliyodidimia. Ugonjwa huu unaweza kuzuiwa kwa kutumia mbegu zilizothibitishwa kitaalamu, kubadilisha mazao na kuepuka kujeruhi karoti wakati wa kupalilia, kuvuna au kusafirisha.
Wadudu:
· Minyoo Fundo:
Minyoo hii hushambulia mizizi na kuifanya iwe na vinundu. Hali hii husababisha mmea kudumaa na kupunguza mavuno. Minyoo fundo huweza kuzuiwa kwa kubalidilisha mazao. Baada ya kuvuna usipande mazao yajamii ya karoti au mazao yanayoshambuliwa na wadudu hawa. Unawezakupandamazao ambayo bayashambuliwi na minyoo fundo kama vile mahindi. Pia hakikisha shamba ni safi wakati wote.
· Imi wa Karoti:
Mashambulizi hufanywa na funza ambaye hutoboa mizizi. Ili kuzuia wadudu hawa tumia dawa kama vile Dichlorvos, Sapa Diazinon na Fenvalerate. Pia badilisha mazao na wakati wa kupalilia pandishia udongo kufunika mizizi.
· Karoti Kuwa na Mizizi Mingi (Folking);
Hii hutokea kama karoti zimepandwa kwenye udongo wenye takataka nyingi na usiolainishwa vizuri. Vile vile utumiaji wa mbolea za asili zisizooza vizuri unaweza kusababisba karoti kuwa na mizizi mingi. Hali hii inaweza kuzuiwa kwa kulainisha udongo vizuri na kutumia mbolea za asili zilizooza vizuri.
Mavuno
Karoti hukomaa siku 90 hadi 120 baada ya kupanda kutegemea na aina ya mbegu na hali ya hewa. Wastani wa mavuno kwa eka moja ni tani 10 au zaidi ambazo tani kumi hizi ni sawa na kilo 10,000 kwa eka moja.

ASANTE KWA KUFUATILIA BLOG YETU 
KARIBU KWA SOMO LINGINE SIKU NYINGINE 

5 comments:

  1. ayoo magonjwa yana kingwa na dawa gani

    ReplyDelete
  2. na ombene mnisadie kwa ili coz ni mara ya kwanza nafanya kilimo cha karoti kwenye shamba lenye urefu wa cm 120 na upana wa cm 45 itaingia mbegu kiasi

    ReplyDelete
  3. Ni mbegu gani bora na inayovumilia magonjwa

    ReplyDelete
  4. Wastani wa bei kwa gunia 1 la karoti ni Tsh.ngapi?

    ReplyDelete